Decoration & Catering Services

Decoration & Catering Services

Boutique

Boutique

Thursday, August 22, 2013

Profesa Senzota wa UDSM, mbaroni kwa kujeruhi kwa risasi

Professa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ramadhani Senzota, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kumjeruhi kwa risasi fundi ujenzi, aliyefahamika kwa jina la Fadhili Mkachini.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 10:50 jioni eneo la Tegeta Salasala, wakati Fadhili na mafundi wenzake wakiendelea na ujenzi.

Kamanda Kova alisema tukio hilo lilitokea baada ya mafundi hao wakiendelea na ujenzi wa nyumba ya mtu anayetambulika kwa jina la Khadija, ndipo Profesa huyo alitokea na kuwataka wasitishe shughuli hiyo.

Kova alisema kabla ya mafundi hao kufanya chochote, Profesa huyo alichomoa bastora aina ya Akidali Mini yenye namba 03 TZ CR 92277, iliyokuwa na risasi saba ndani ya magazine na kumpiga fundi huyo tumboni na kumsababishia maumivu makali.

Hata hivyo, Profesa Senzota anashikiliwa na polisi kwa upelelezi zaidi na fundi huyo amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala akipatiwa matibabu.

Wakati huo huo, watu saba wanaosadikiwa kuwa majambazi wanashikiliwa na Polisi kwa kufanya uhalifu wa kutumia silaha, sare za polisi na redio ya mawasiliano katika maeneo ya Boko, Tegeta, Mbweni, Bahari Beach na maeneo mengine ya Jiji.

Watuhumiwa hao ni Khamis Mkalikwa (40), Magila Werema (31), Nurdin Bakari (46), Materu Marko (32), Louis Magoda (34), Amos Enock (23) na Amir Mohamed (45), wote wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Kamanda Kova alisema watuhumiwa hao walikamatwa jana katika eneo la Kiluvya, Wilaya ya Kinondoni na walikuwa wakitumia gari aina ya Toyota Cresta GX 100, yenye namba za usajili T 546 BWR.

Baada ya kukamatwa watuhumiwa hao walikutwa na bastora moja aina ya Brown B.3901, ambayo ilikutwa na risasi nne na ganda moja la risasi, sare za polisi pea mbili na moja yenye cheo cha Stesheni Sajenti na nyingine ikiwa na beji inayosomeka kwa jina la SSGT A.M.Mduvike.

Kova alisema watuhumiwa wawili kati ya saba wamejeruhiwa na wapo hospitali kwa matibabu na uchunguzi dhidi yao bado unaendelea.

Katika tukio lingine, mtu aliyetambulika kwa jina la Alquine Masubo (42), anashikiliwa na polisi kwa kosa la kujifanya Ofisa Usalama wa Taifa.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa na vielelezo mbalimbali ikiwamo kitambulisho cha JWTZ namba 7001-E.1075, bastola aina ya Browning yenye namba A.956188-CZ83 ikiwa na risasi 12 ndani ya magazine, pia alipekuliwa nyumbani kwake na kukutwa na bastola nyingine aina ya MAKNOV yenye namba BA4799 ikiwa na risasi 19 na bastola moja ilikuwa na umiliki na nyingine ilikuwa haina.

0 comments:

Post a Comment