Decoration & Catering Services

Decoration & Catering Services

Boutique

Boutique

Wednesday, August 21, 2013

HATARI ZIWA VICTORIA



Picha hii inaonesha mfereji (kulia) unaotoka Soko Kuu la Mji wa Bukoba ukiwa umebeba vinyesi kutoka maeneo mbalimbali likiwemo Gereza la Bukoba, Uchafu unaotoka katika gereza hilo hupitia Shule ya Msingi Rumuli kabla ya kuungana na mfereji huo ambao hukutana na Mto Kanoni, kama inavyoonekana pichani.

 
Kwa kweli hakuna moyo wa uzalendo katika suala la kutunza mazingira ya Ziwa Victoria, kama leo hii ukiwauliza Magereza taka ngumu na kinyesi wanamwaga wapi, huwezi kupata jibu, wanarukaruka tu,” Magongo- Mfuatiliaji na Mtathmini Mradi wa KADETFU 

SERIKALI imeweka sheria mbalimbali zinazolenga kutunza mazingira ikiwemo Sheria ya Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004
.Pia mwaka 2009, Serikali ilipitisha Sheria Namba 11 ya rasilimali za maji na Sheria Namba 12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ambazo kwa pamoja zinalenga kulinda na kutunza nyanzo vya maji.
 
Sheria hizi zinatoa adhabu, mfano katika kifungu cha 52(1) cha Sheria Namba 12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, kinatoa faini ya kiwango cha shilingi milioni moja au kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja kwa mtu yeyote atakayesababisha uchafuzi wa chanzo cha maji. 

 

Hata hivyo, licha ya kuwepo sheria hizo bado kumekuwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria unaofanywa na wananchi, viwanda, mahoteli pamoja na taasisi mbalimbali za serikali na zile zisizo za Kiserikali. 

Jeshi la Magereza mjini Bukoba Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa taasisi za umma ambazo kwa kiasi kikubwa zinadaiwa huwa zinahusika katika kuchangia kuchafua mazingira ya Ziwa Victoria kupitia utiririshaji wa vinyesi katika Ziwa Victoria. 

Kupitia gereza lililopo Bukoba Mjini, uchunguzi umebainisha kuwa, gereza hilo limekuwa likitapisha kinyesi kwenye mtaro unaotoka katika gereza hilo, ambao unapita nyuma ya mfereji unaokatiza katika Kanisa la Kisabato la Seventh Day Adventist kuja Barabara ya Uganda iliyopo Mtaa wa Rumuli. 

Kinyesi hicho, huwa kinaingia katika mfereji unaotoka katika Shule ya Msingi Rumuli kupitia Soko Kuu na kuungana na Mto Kanoni ambao unapeleka moja kwa moja taka hizo ziwani. 

Katika uchunguzi uliofanywa na Majira katika mfereji unaotoka Shule ya Msingi Rumuli na kuungana na mfereji unaotoka gerezani ni kama mita 200 hadi 300 kuingia ziwani kupitia mto Kanoni ambapo umebainisha utiririshaji wa vinyesi ovyo. 

Uchunguzi huo ulikuwa ni mwendelezo wa kuangalia uchafuzi wa mazingira Ziwa Victoria unaofanywa na Jeshi la Magereza kwa kumwaga vinyesi vya wafungwa na ongezeko la magugu maji ziwani humo. 

Ambapo katika makutano ya mfereji wa Rumuli na gereza, eneo hilo la makutano hayo kumezibwa ili kusiweze kuonekana kwa urahisi wakati wa kutemesha kinyesi hicho. 

Gazeti hili liliweza kufanya uchunguzi na kujionea mtaro ambao uko pembezoni mwa Barabara ya Uganda unaotokea gerezani karibu na Kanisa hilo, ambao ulikuwa ukitiririsha na umejaa maji taka ambayo yalikuwa yakitoa harufu kali, ambayo unaweza kuifananisha na mzoga wa mnyama aliyekufa kwa muda katika maeneo hayo. 

Baada ya kugundua hali hiyo gazeti hili liliweza kufanya mahojiano na baadhi ya wananchi wakiwemo wadau wa mazingira wa maeneo hayo, ambao nao walionesha kuguswa na tatizo hilo. 

Tatizo ambalo wanasema linafanya hali ya hewa kuwa mbaya wakati wa masika, ambapo gereza hilo hutumia mwanya huo kutapisha kinyesi hicho jambo ambalo linaleta usumbufu mkubwa kwa wakazi hao. 

WANANCHI WANENA 

Mmoja wa waumini wanaosali katika Kanisa la Wasabato la Seventh Day Adventist ambaye alijitambulisha kwa jina la Editha Rweyimamu anasema, harufu mbaya inayotoka gerezani hapo hasa wakati wa mvua imekuwa ikisababisha waumini kushindwa kupata usikivu wa neno la Mungu pindi wanapokuwa kwenye ibada. 

“Wakati huu wa kiangazi hali kidogo huwa shwari (nzuri), lakini maji taka hayo huwa wanatiririsha kidogo sana ila wakati wa mvua unashindwa hata kutafakari hii harufu ni ya kitu gani, kwa maana harufu huwa ni nzito na inaenea kanisa zima,” alisema Rweyimamu. 

Naye Jumanne Issa ambaye anajihusisha na biashara ya kuuza vitabu kwenye eneo hilo kwa miezi nane sasa anasema, amekuwa akishuhudia harufu ya vinyesi kutoka katika mfereji unaotoka gerezani, huku kila mtu anayepita karibu na mfereji huo akilazimika kufunga pua. 

Wakati mwananchi huyo akisema hivyo, mwandishi wa makala haya alifanikiwa kupita kila eneo ambalo linazunguka Gereza na kushuhudia maji taka hayo yakitiririka kutoka mfereji wa Gereza kupitia Barabara ya Uganda, ambayo yanakutana na mfereji wa Shule ya Msingi Rumuli na kuingia Mto Kanoni, ambao unapeleka maji moja kwa moja ziwani. 

“Harufu inatuathiri sana, tunashangaa kuona serikali imelifumbia macho, tunaomba watafute njia ya kumwaga kinyesi hicho sio kupeleka ziwani mahali ambapo tunapata chakula na maji ya kunywa,” alisema muuza vitabu huyo. 

WADAU WA MAZINGIRA 

Wakizungumzia suala hilo kwa nyakati tofauti, wadau wa mazingira katika Manispaa ya Bukoba nao walisema kuwa, gereza hilo limekuwa likitiririsha kinyesi mwaka mzima mfululizo na kuingiza Mto Kanoni ambao unapeleka maji ziwani.

Michael Cleophans ambaye ni katibu mkuu wa taasisi inayojishughulisha na masuala ya mazingira ya Envirocoment mjini Bukoba anasema, gereza hilo limekuwa likitiririsha kinyesi kupitia mfumo ambao si rasmi wa kunyonya vyoo vilivyotitia, yakiwemo maji taka kutoka kwenye vyumba vya wafanyakazi na kuyatiririsha kwenye mfereji kupitia kanisa hilo la Wasabato. 

Anasema, suala hilo wamekuwa wakilijadili mara kwa mara katika vikao vyao vya mazingira, lakini limekuwa likichukuliwa sana kisiasa. 

“Kutokana na vitisho vikali kutoka kwao (gereza), watu wamekata tamaa na taasisi zingine za kiserikali zinazoshughulika na mazingira, walisema watalifuatilia, lakini hadi leo (mwishoni mwa wiki) zimeendelea kuwa kimya,” anasema mdau huyo. 

Aidha, anasema kuwa pamoja na kwamba hakuna miundombinu ya mfumo wa maji taka katika Manispaa ya Bukoba isiwe sababu ya wao kukwepa gharama za kulipia magari ya kunyonya maji taka hayo na kuyapeleka kumwaga katika eneo ambalo limetengwa na Manispaa kwa ajili hiyo. 

Naye Justus Magongo ambaye ni Mfuatiliaji na Mtathmini Mradi katika Shirika la Maendeleo Kagera (KADETFU) anasema kuwa, taasisi nyingi katika Manispaa ya Bukoba ikiwemo Magereza zinahusika katika uchafuzi wa mazingira kutokana na ukosefu wa miundombinu. 

Anasema kuwa, wao kama taasisi isiyo ya kiserikali wanafanya kazi pale ambapo serikali haiwezi kufika.

“Tumeweza kufanya semina kwa viongozi wa taasisi mbalimbali na Magereza wakiwemo, ili kutoa hamasa katika kupunguza tatizo hili, lakini cha ajabu hakuna utekelezaji wowote uliofanyika. 

“Kwa kweli hakuna moyo wa uzalendo katika suala la kutunza mazingira ya Ziwa Victoria, kama leo hii ukiwauliza Magereza taka ngumu na kinyesi wanamwaga wapi huwezi kupata jibu wanaruka ruka tu,” anasema Magongo. 

MRADI WA LVEMP II 

Mratibu wa Mradi wa Ziwa Victoria Awamu ya Pili (LVEMPII) Manispaa ya Bukoba, Richard Salu alikiri kufahamu kuwa kuna mtaro unaotoka Magereza kuingia Mto Kanoni unaotiririsha uchafu ingawa bado hawajajua ni uchafu wa kiasi gani ambao unaingizwa ziwani. 

“Nafahamu sana, ila hiki ni kituo cha serikali, hivyo pindi itakapobainika tutakaa nao meza moja ili kuwashauri maji taka hayo yaweze kutibiwa kabla hayajaingia ziwani au waunganishe kwenye mfumo wa maji taka wa manispaa ambao bado haujajengwa,” anasema Salu. 

Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili ulibainisha kuwa licha ya kutokuwepo kwa mfumo wa maji taka katika mji wa Bukoba mkoani Kagera, Manispaa imetenga eneo la Nyanga nje kidogo ya mji huo kwa ajili ya kumwaga huo uchafu, lakini watu wamekuwa hawatumii, badala yake wamekuwa wakisubiria mvua ikinyesha waruhusu kinyesi hicho kiweze kutapishwa. 

OFISA MAZINGIRA BUKOBA 

Ofisa Mazingira katika Manispaa ya Bukoba , Hamza Kambuga alipohojiwa kuhusiana na suala hilo alikiri Magereza kutapisha kinyesi, japo kuwa wana makaro ya maji taka ambayo yanadaiwa huwa yanazidiwa kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wafungwa. 

Anasema kuwa, wakati gereza linajengwa (mwaka 1937) lilikadiriwa kuwa na wafungwa wachache ( wafungwa 360) hivyo gereza lilikuwa dogo. 

Kwa kuwa, wakati huo ilikuwa ni ngumu kujenga mfumo wa maji taka mkubwa wa kiasi hicho kama inavyohitajika hivi sasa, hivyo tangu wakati huo mfumo wa gereza haujapanuliwa na miundombinu iko vilevile na wafungwa wakizidi kuongezeka. 

Anasema kuwa, tatizo hilo wanaliona lakini changamoto yake ni kubwa hali hiyo inaweza kutatuliwa endapo mfumo wa maji taka utajengwa ambapo wataweza kuunganisha moja kwa moja. 

Hata hivyo, Kamishna Msaidizi wa gereza hilo, ACP Nkonjelwa alipohojiwa na mwandishi wa makala hii juu ya idadi ya lini gereza hilo lilianzishwa na idadi ya wafungwa kipindi hicho hadi leo alisema kwa kifupi; “ lilianzishwa mwaka 1937, likiwa na uwezo wa kuchukua wafungwa 360, kwa sasa hivi wapo 437 ambapo wafungwa ni 213 na mahabusu 224,” alisema ACP huyo. 

MAABARA BUKOBA 

Gazeti hili liliweza kuonana na Mkuu wa Maabara katika Manispaa ya Bukoba, Marco Vitta ambaye alithibitisha kuwa, gereza hilo limekuwa likihusika katika utapishaji wa kinyesi hicho ziwani (kupitia maeneo ambayo yametajwa hapo juu). 

Anasema kuwa, kwenye kipindi cha mvua maji taka hayo yanakuwa hayaonekani moja kwa moja kutokana na kinyesi hicho kuchukuliwa na maji moja kwa moja ila wakati wa kiangazi hali inakuwa ni mbaya zaidi, vinyesi vinakuwa vinatapakaa. 

Anasema kuwa, mwanzoni hali hiyo haikuwa mbaya sana katika kipindi cha nyuma kutokana na Magereza kutokuwa na wafungwa wengi, lakini hali imekuja kubadilika hivi karibuni katika miaka ya 2000 hali hii inaonesha kuwa gerezani kuna msongamano wa wafungwa. 

“Huenda hapo awali katika kipindi cha nyuma, Magereza ilikuwa ikitapisha kwa mwaka mara moja kutokana na idadi ndogo ya wafungwa waliokuwepo (360), lakini hivi sasa kutokana na wingi wa wafungwa unakuta ‘septic’ (mfumo wa maji taka) zinajaa ndani ya miezi mitatu hadi nne hivyo wanachofanya ni kutapisha kinyesi,” anasema Vitta. 


Anaongeza kuwa, suala hili la gereza kutapisha kinyesi ziwani limekuwa ni gumu kupatiwa ufumbuzi kutokana na kwamba hiyo ni taasisi ya kiserikali. 

“Hivyo ni jukumu la serikali kulitafutia suluhu japo hili, vipimo vya kimaabara vinavyofanyika kila mara kwa maabara kuchukua sampuli za majitaka hayo kutoka Magereza zinaonesha maji taka yanayotiririshwa kutoka kwao ni kinyesi kitupu,” anasema Mtaalamu huyo. 

MKUU WA MAGEREZA 

Gazeti hili lilimtafuta Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kagera (RPO) ambaye pia ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza Mkoa wa Kagera, Yusuph Kimanji (amestaafu tangu Julai Mosi, mwaka huu) ili aelezee suala hili kwa upana zaidi. 

Mkuu huyo, alidai kuwa Manispaa ya Bukoba imekuwa ikishindwa kuweka mkakati wa muda mfupi na mrefu wa jinsi gani ya kuwa na mfumo wa maji mjini Bukoba. 

“Jambo hili (kutiririsha vinyesi ziwani) si kweli, wanaisema Magereza kwa sababu wanaichukia taasisi hii, lakini ukweli ni kwamba maji taka katika majengo yote Bukoba yanapita katika Mto Kanoni na kuingia ziwani,” anasema Mkuu huyo wa gereza. 

Alipoulizwa kuhusiana na maji taka yanayotiririka kutoka kwenye gereza hilo, alikana na kusema kuwa wao hawahusiki na utiririshaji wa maji taka. 

“Kama tungefanya hivyo, tusingehusika katika kuombea fedha suala la kunyonya maji taka toka serikalini.

“Tangu nimeingia katika ofisi hii mwaka 2007, mwezi Julai niliona kuna matatizo ya mfumo wa maji taka, katika mji wa Bukoba na ndio maana niliamua kuweka utaratibu wa kuombea fedha jambo hili,” anasema Kimanji. 

Hata hivyo, alimuonesha mwandishi wa makala hizi nyaraka ambazo zinazoonesha fedha walizoomba katika kupindi cha mwaka 2010/2011 ambapo walipokea sh. milioni 6.5. 

Mwaka 2011/2012 zilikuwa ni sh. milioni 7.1 ambazo zote zilikuwa kwa ajili ya kunyonya maji taka kutoka katika maeneo ya Magereza na mwaka 2012/2013 walipokea sh. milioni 5.6. 

Fedha ambazo zilikuwa kwa ajili ya kukarabati mfumo wa maji taka ambao bado wanautekeleza ili kuhakikisha kuwa hakuna maji yanayopotea na kwenda kuzagaa nje. 

Alipoulizwa kuhusiana na hali aliyoikuta wakati anakabidhiwa gereza hilo, Mkuu huyo alikataa kuzungumza na kudai kwamba hawezi kuongelea masuala ya nyuma kwani kwa wakati huo hakuwepo na hawezi kujua kilichokuwa kinaendelea. 

“Sitaki kuongelea suala hilo, ila anayestahili kubeba lawama ni manispaa, kwa nini haina nfumo wa maji taka na pia haina magari ya kunyonya maji taka na badala yake tunaenda kukodi magari ya watu binafsi,” anasema Kimanji. 

Katika kuthibitisha kauli yake kuwa, hawamwagi kinyesi ziwani kupitia Mto Kanoni, gazeti hili liliamua kuwatafuta madereva waliopewa dhamana na Manispaa ya Bukoba ya kunyonya maji taka katika mji huo ili waweze kuthibitisha kama huwa wanatumiwa na taasisi hiyo ya Magereza ili kunyonya maji taka na vinyesi.

Lengo ni kutaka kujua kama ni kweli Magereza hawahusiki au katika uchafuzi wa ziwa na pia kuhakikisha kama kweli fedha ambazo wanaletewa na serikali kwa ajili ya kunyonya maji taka kama zinatumika ipasavyo kama alivyosema. 

SAUTI ZA MADEREVA 

Miongoni mwa madereva ambaye hakutaka kutaja jina lake na kampuni anayoiwakilisha gazetini kwa kuhofia kupoteza wateja wake alimweleza mwandishi kuwa, taasisi hiyo ya Magereza huwa inawakodi kunyonya maji taka kwa mwaka mara moja.

“Ni kutoka katika makaro ya magereza hiyo,” anasema Dereva huyo. 

Anasema kuwa, mara ya mwisho kukodiwa na magereza ilikuwa ni Oktoba, mwaka jana hadi leo hii hawajawahi kukodiwa. 

Pia Dereva huyo anasema kuwa, pindi wanapokodiwa huwa wanapewa mkataba wa kubeba awamu 10 ambapo wao wanachaji kila moja sh. 120,000. 

Anasema kuwa, maji taka hayo huwa wanayanyonya katika makaro matano yaliyopo katika gereza hilo na pindi wanapokuwa wananyonya huwa wanapunguza punguza kutoka katika karo moja na huwa hawatoi yote ili kuhakikisha tripu 10 zinatimia na mengine yanayobaki wakati wa mvua Magereza wenyewe huwa wanatapisha katika mtaro, kwa kutumia ndoo ambapo kazi hiyo hufanywa na wafungwa. 

“Mwaka huu tangu uanze hatujawahi kukodiwa na Magereza, mara ya mwisho wametukodi mwaka jana mwezi Oktoba na huwa wanatukodi mara moja kwa mwaka ambapo huwa wanatupa mkataba wa tripu 10 tu, ambazo huwa tunapunguza punguza kutoka katika makaro ya gereza hilo,” anasema Dereva huyo. 

Kutokana na maelezo ya dereva huyo anasema kuwa, kila tripu moja huwa wanatoza sh. 120,000 hivyo kwa tripu 10 ni sawa na shilingi milioni 1.2 ndizo ambazo zinatumika kutoka katika fedha ambazo Mkuu wa Magereza Bukoba alizitaja. 

Kwa kuwa, wanapatiwa kutoka serikalini kila mwaka jambo ambalo linaonesha kuwa hazitoshelezi katika kukidhi mahitaji ya unyonyaji taka na yale yanayobaki kwenye septank yanasubiri kutapishwa wakati wa mvua kama ilivyothibitishwa na dereva huyo. 

WAHUSIKA NA WALINZI ZIWANI 

Mratibu wa Mradi wa Mazingira wa Ziwa Victoria Awamu ya Pili (LVEMPII), Omary Mwamuyanza anasema kuwa ni kweli Magereza huwa wanamwaga kinyesi cha wafungwa ziwani japo si peke yao wako wengi. 

Anasema kuwa, wao kama mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa Victoria pamoja na kujua kuwa Magereza na taasisi nyingine zinachafua mazingira hawana mamlaka ya kuwachukulia hatua bali huwa wanawaeleza manispaa ili watekeleze suala hilo. 

“ S i s i h a t u n a s h e r i a y a kuwachukulia hatua ila watu kama NEMC (Baraza la Mazingira nchini) na Manispaa ndizo ambazo zinatakiwa kutusaidia katika suala zima la kuwachukulia hatua, sisi tunasaidia katika kutekeleza mradi ikiwa ni pamoja na kujenga mfumo wa maji taka katika mji huo ambao utagharimu zaidi ya dola milioni1.5, ambao utakamilika ndani ya miezi 18 ijayo,” anasema Mwamuyanza. 

Anasema kuwa, uchafuzi wa mazingira ya Ziwa Victoria bado ni changamoto kubwa kwani wananchi pamoja na taasisi nyingi hawako tayari kubadili tabia za kutiririsha vinyesi ziwani hadi inawalazimu mara kwa mara kuwaelimisha na mradi unatumia gharama nyingi, lakini hawako tayari kupokea ushauri. 

MSIMAMO WA NEMC 

Gazeti hili lilimtafuta Mratibu wa Kanda ya Ziwa katika Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Anna Mdamo ambaye ofisi zake zipo jijini Mwanza ili aweze kujibu ni kwa nini Gereza la Bukoba limekuwa likichafua ziwa kwa kumwaga kinyesi cha wafungwa ziwani na sheria za kulinda mazingira zikiwepo.

Mdamo alisema kuwa, wao kama kanda hawajathibitisha kama Magereza wanachafua ziwa alisema kuwa, mtu anayetakiwa kuthibitisha kuwa Magereza wanachafua ziwa kwa kumwaga kinyesi ziwani ni Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Bukoba.

“Sina taarifa zozote kuhusiana na gereza kutiririsha kinyesi ziwani, hatujafanyia kazi na wala hatujaletewa malalamiko, ila pindi tutakapoambiwa na kuthibitisha kuwa wanahusika katika suala zima la uchafuzi wa mazingira tutaenda kuonana nao na kuwachukulia hatua,” aliongeza. 

Uchunguzi unaonesha kuwa, uchafuzi wa mazingira ndani ya Ziwa Victoria unaofanywa na wananchi zikiwemo taasisi mbalimbali za serikali hasa Gereza la Bukoba kwa kutirisha kinyesi ziwani ni tatizo ambalo linaathiri watumiaji wa ziwa pamoja na viumbe hai kwa ujumla.

Inakadiriwa kuwa, ziwa hilo linategemewa na wakazi zaidi ya milioni 35 kutoka nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi ambapo ziwa hilo lina ukubwa wa mita za mraba 194,000 huku Tanzania ikimiliki asilimia 44 ya eneo lake lote.

0 comments:

Post a Comment