Rais Kagame
Kwa muda wa miezi takriban minne kumekuwa na
maneno ya kejeli kutoka kwa Serikali ya Rwanda na kwa hakika maneno hayo
yanatoka mdomoni mwa Rais Paul Kagame na maofisa wa ngazi za juu katika
Serikali yake.
Kagame amekuwa mbogo baada ya Rais Jakaya Kikwete
kumshauri afanye mazungumzo na wapiganaji wa Kihutu waliokimbilia
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) baada ya kutuhumiwa kufanya mauaji
ya kimbari nchini mwake mwaka 1994.
Inakadiriwa kuwa Watutsi na Wahutu 800,000 wenye
msimamo wa wastani waliuawa wakati huo, ingawa takwimu hizo zina utata,
kwani wako wanaodai kuwa nchi hiyo wakati huo ilikuwa na idadi ndogo ya
watu ambao idadi hiyo inasemekana ndio waliouawa.
Pia, wapo wale ambao wanaweza kushangaa kwa nini
Kagame amekuwa hivyo na kuikosea heshima Tanzania, nchi ambayo imekuwa
mstari wa mbele kupokea wakimbizi wake toka miaka ya 1960 na kwa nini
Rais Kikwete alitoa ushauri huo.
Kagame hakupendezwa na ukweli huo kwani kila mara
amekuwa akikataa kuwa hana mkono katika mapigano yanayoendeshwa na
vikundi vya msituni vinavyoanzishwa nchini DRC kila inapotokea hali
kutulia.
Kikwete amekuwa akijua jambo hili kwa muda mrefu
kwani amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa kipindi cha miaka kumi na
amekuwa akihudhuria mikutano ya kutafuta amani ya DRC bila mafanikio kwa
sababu kila kikundi kinapoingizwa katika jeshi la DRC na kudai kuwa
kimemaliza vita kinazuka kikundi kingine ambacho nacho kinaanzisha
mapambano dhidi ya serikali.
Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa
Mataifa (UN) alikuwa mkuu wa shughuli za kijeshi za umoja huo kabla
hajapanda cheo na kuwa katibu mkuu wa umoja huo, alipotembelea Rwanda
baada ya kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, msafara wake
ulirushiwa nyanya.
Hiyo ilikuwa ni kama kumpa ujumbe kuwa hakuna alichofanya wakati ule Watutsi walipouawa na Wahutu mwaka 1994.
Masikini! Annan angefanya nini wakati alipokuwa
akiyaomba mataifa makubwa kuingilia kati ili kusitisha mauaji kila moja
lilikuwa likiangalia maslahi yake na ulikuwepo mpango wa uchelewashaji
wa makusudi.
Baadaye Annan alipokuwa akigombea Ukatibu Mkuu wa
UN ni Rwanda pekee katika nchi za Afrika ndiyo iliyopinga na hata
alipokuwa akiomba kuongezewa muda ni nchi hiyo iliyokuwa kinara wa
kumpinga wakati ukweli ni kuwa mambo yote yaliyokuwa yakifanyika wakati
huo Kagame alikuwa akiyajua.
Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Rwanda, Meja Jenerali
Kayumba Nyamwasa, alinukuliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza
(BBC) akiwa uhamishoni Afrika Kusini akithibitisha kuwa vikundi vyote
vimekuwa vikianzishwa na Kagame kwa nia ya kuhakikisha kuwa Wahutu na
jeshi la zamani la nchi hiyo ambalo kwa sehemu kubwa linaundwa na
waliokuwa vijana wa Inteharamwe hawapati muda wa kujijenga.
0 comments:
Post a Comment