Mshambuliaji wa Yanga Haruna Niyonzima (katikati) akiwania mpira na
wachezaji wa Coastal Union, Jerry Santo (kulia) na Uhuru Seleman
(kushoto) wakati wa mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam jana. Matokeo sare ya 1-1
Bao la ‘usiku’ lililotokana na kiki ya penalti liliiokoa kipigo Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga na kufanya matokeo kuwa sare ya bao 1-1, huku Simba ikizinduka kwa Oljoro ya Arusha na ushindi kiduchu wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abied Arusha katika mechi ya raundi ya pili ya michuano hiyo.
Kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, kulikuwa na
kila dalili Yanga kuchomoka na pointi tatu mpaka dakika ya 90, Coastal
waliposawazisha kwa penalti ya Jerry Santo baada ya David Luhende
kuucheza mpira kwa mkono ndani ya boksi lake la hatari.
Mechi hiyo ya kupendeza na ushindani mkali,
ilishuhudia pia kadi mbili nyekundu kwa kila upande na idadi kubwa ya
kadi za njano zilizolalamikiwa na Kocha wa Yanga, Ernie Brandts.
Awali, Yanga iliyoanza ligi kwa ushindi mnono wa
mabao 5-1 dhidi ya Ashanti United wiki iliyopita, walitangulia kufunga
kupitia kwa mshambuliaji Didier Kavumbagu katika dakika ya 70.
Wageni Union walikuwa wa kwanza kulitia msukosuko
lango la Yanga mapema katika dakika ya kwanza baada ya Uhuru Seleman
kuchomoka na mpira kwa kasi na kumimina krosi iliyomalizwa vibaya na
Chrispine Odula.
Yanga ilijibu shambulizi dakika ya nane baada ya
Simon Msuva kushindwa kufunga na badala yake akampasia mpira kwa kichwa
kipa wa Coastal Shaban Kado kutokana na krosi ya Salum Telela.
Dakika ya 24, Union walifanya shambulizi kali
langoni kwa Yanga na kumlazimu kipa Mustapha kujinyoosha na kupangua
shuti kali la Tutimba na kuwa kona iliyokosa ‘mazao’.
Tegete alishindwa kulenga lango la Coastal baada
ya shuti lake nje ya 18 kupaa juu ya lango la Yanga, huku Wagosi wa Kaya
nao wakishindwa kufunga kwa staili hiyohiyo kupitia kwa Odula.
Katika mchezo huo uliomaliza dakika 45 za kwanza
bila bao, mwamuzi Martin Saanya aliwaonyesha kadi nyekundu wachezaji,
Odula na Msuva kwa kosa la kusukumana.
Saanya pia aliwaonyesha kadi za njano wachezaji
Juma Nyoso, Seleman Kassi wa Coastal Union, huku Didier Kavumbagu,
Telela, Niyonzima na Msuva wakionyeshwa kwa upande wa Yanga.
0 comments:
Post a Comment