Hatimaye vikosi vya usalama
nchini Kenya vinasema vimelidhibiti jengo zima la Westgate mjini
Nairobi, ikiwa ni zaidi ya siku tatu baada ya jengo hilo kuvamiwa na
wanamgambo.
Milipuko ikifuatiwa na milio ya risasi imesikika
kutoka ndani ya jengo hilo asubuhi ya leo huku duru zikisema kuwa
vikosi vya usalama vinaelekea kukamilisha operesheni hiyo.Serikali imesema zaidi ya watu 60 wameuawa na wengine zaidi ya 170 kujeruhiwa katika shambulio hilo ambalo Al shabaab imekiri kulitekeleza.
Wizara ya mambo ya ndani imesema wanajeshi wanaendelea kulisaka jengo zima la Westgate kutoka orofa moja hadi nyengine kuhakikisha kwamba hakuna mateka aliyesalia.
Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje amesema kuwa wawili kati ya wanamgambo watatu waliofanya shambulii hilo ni raia wa Marekani pamoja na mwanamke muingereza.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani, Amina Mohamed alisema kuwa wamarekani walikuwa kati ya umri wa miaka 18 na 19 ingawa wenye asili ya kisomali au kiarabu na waliishi mjini Minnesota. Mshukiwa mwingine alikuwa mwanamnke Muingereza ambaye inasemekana alikuwa amefanya vitendo vingi vya aina hii kwa niaba ya Al Shabaab.
Kundi la kigaidi la al-Shabab limekiri kutekeleza mauaji hayo, kulipiza kisasi hatua ya Kenya kujihusisha kijeshi nchini Somalia.
Operesheni hiyo iliendelea usiku kucha ingawa kwa mujibu wa waziri wa usalama wa Kenya, ilikuwa katika mkondo wake wa mwisho.
"magaidi hawa huenda wanakimbia na kujificha katika sehemu mbali mbali za jengo hilo lakini ghorofa zote za jengo hilo zimedhibitiwa na majeshi,'' alisema Ole Lenku. Aliongeza kuwa mateka wote walifanikiwa kuokolewa.
Jumatatu jioni moshi mkubwa ulionekana ukifuka kutoka kwenye jengo la Westgate ukiambatana na moto mkubwa. Moto huo unasemekana uliwashwa na wanamgambo hao ili kutatiza vikosi vya usalama katika juhudi zao za kutaka kukomboa jengo hilo.
0 comments:
Post a Comment