Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
WAKATI leo ndiyo siku ya mwisho Ikulu kupokea mapendekezo ya majina kutoka kwa makundi mbalimbali, tayari makundi yapatayo 50 yamewasilisha mapendekezo ya majina ya watu ambao wangependa wawe wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Makundi hayo ni asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya Serikali, vyama vya kitaaluma, madhehebu ya dini na vyama vya siasa ambayo jumla yanafanya idadi hiyo kuwa 50 na inatarajiwa kuongezeka leo kutokana na makundi mengine kuwasilisha majina leo.
Taarifa iliyotolewa juzi Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ilieleza kuwa taasisi hizo zimewasilisha majina yao kwa mujibu wa mwaliko uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete ili kukidhi Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Sheria hiyo sura ya 83 Kifungu cha 22(1) (c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinataka makundi kupendekeza majina na kuyawasilisha kwa Rais ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kufanya uteuzi wa wajumbe wa Bunge la Katiba.
Taarifa hiyo ilifafanua, kuwa makundi hayo 50 yaliyowasilisha majina yanayopendekezwa yanatokana na barua 169 zilizopokewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar.
Makundi ambayo yamewasilisha majina kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Shirika la Wasaidizi wa Jamii Kabila la Wagogo, Tanzania Association of Social Workers (TASOWA), Jukwaa la Walimu na Wanafunzi Tanzania, Chama cha Walimu Wanawake Tanzania, Umoja wa Wanawake Wajane wa Wilaya ya Karagwe na Kyerwa (UWK).
Mengine ni Tanzania Peace and Development Society, Better World Organization (BWO), Youth Focus and Development, Association of Traditional Medicine Man, Registered Centre for Good Governance and Development in Tanzania, Chama Cha Kijamii (CCK), CHANETA na Muungano wa Wanajeshi Wastaafu Tanzania.
Makundi mengine ni Legal Aid Iringa Village, Tanzania Kilolo Orphans and Social Development Organization, Legal Aid and Social Welfare Association, Legal and Human Right Centre, Tanzania Lift Initiative NGO, Kilolo Paralegal Unit, Women Development and Social Activities Association, Defence of Human Right/Citizen Rights.
Pia kuna makundi ya DAWSEN Trust Fund, Baruti Development Association (BADEA), Living Hope Ministries Trust, EFATHA Ministry, Bethel Assemblies of God Tanzania, Muslim and Christian Brotherhood Society, Baraza Kuu la Waislamu wa Kondoa – Tanzania na Jesus Temple Inner Transformation News.
Zingine ni Jumuiya ya Waithna Asharriyyah Tanzania, Rehmatfi Sabilillah Trust of Tanzania, Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), National Reconstruction Alliance (NRA), Sauti ya Umma (SAU), Chama cha Demokrasia Makini, African Progressive Part – APPT Maendeleo, National League for Democracy, Tanzania Film Federation, Taasisi ya Maendeleo ya Utamaduni, Al-Amoud General Enterprises.
Taarifa hiyo ilitaja makundi mengine kuwa ni Blue Belt and Water Sources Control, Community Development Training Institute – Tengeru, Tanzania Medical Student Association, Tanzania Sea Farmers Union, Medical Association of Tanzania, Chama cha Wastaafu wa Mbinga, Union of Tanzania Press Clubs, Umoja wa Wanawake Tanzania, Alliance for Tanzania Farmers Party na Tanzania Social Economic and Environment and Wellbeing.
Taarifa ya Ikulu ilisema kwa vile mwisho wa kupokea orodha ya majina hayo ni leo, Balozi Sefue alitoa mwito kwa makundi mengine ambayo hayajawasilisha orodha hiyo kufanya hivyo kabla muda uliowekwa kwisha.
Aidha, taarifa hiyo ilitaka makundi hayo kuwa wakati wa kuwasilisha majina hayo ni muhimu kuzingatia vigezo vilivyowekwa na sheria na kama vilivyofafanuliwa kwenye Tangazo la Serikali Namba 443 lililochapishwa Desemba 13, mwaka jana.
Wakati anatoa salamu zake za Mwaka Mpya kwa Taifa juzi, Rais Kikwete alisema mchakato wa kupata wajumbe 201 watakaoungana na wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunda Bunge Maalumu la Katiba umeanza.
Alisema ni matarajio yake kuwa katika wiki ya tatu ya mwezi huu, uteuzi utakamilika. Siku 21 baada ya hapo Bunge la Katiba litaanza. Hii ni kwa nia ya kuwapa nafasi wajumbe hao kusoma Rasimu ya Katiba. Chadema leo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitawasilisha mapendekezo yao ya majina leo baada ya kupokea maombi mengi kutoka kanda zote 10 zinazohusisha mikoa, wilaya na majimbo.
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano, John Mnyika ilieleza kuwa baada ya Ikulu kutoa tangazo la kutaka makundi kuwasilisha majina hayo, chama hicho kilitoa mwito kwa wanachama wake ambao wangependa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba kuwakilisha CHADEMA, watume maombi makao makuu ya chama na katika ngazi nyingine husika.
“Maombi yamekuja mengi kutoka kanda zote 10 za chama zinazohusisha mikoa, wilaya na majimbo nchini. Sekretariati ya chama, jana ilianza vikao vya kupitia majina hayo, kazi inaendelea tena leo (jana)", ilisema taarifa hiyo. Mnyika alisema baada ya uchambuzi huo, chama kitawasilisha majina hayo kama matakwa ya sheria na tangazo la Rais yanavyohitaji.
0 comments:
Post a Comment