Kamishna wa Polisi, Ernest Mangu.
Juzi, Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete, alimwapisha Ernest Mangu kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) akichukua nafasi iliyoachwa na Said Mwema ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria.
Mbali na Mangu, Rais pia alimwapisha Abdulrahman Kaniki kuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, cheo kipya katika mfumo wa jeshi hilo. Tunapenda kuwapongeza makamanda hao wawili kwa uteuzi huo, pia kumtakia heri ya kustaafu, Mwema.
Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo, tunaamini kwamba wanazifahamu vyema changamoto zinazowakabili katika kutimiza majukumu yao hasa ikizingatiwa kwamba ‘wamekulia’ ndani ya jeshi hilo.
Mara baada ya kuapishwa, Mangu alikaririwa na vyombo vya habari akisema kwamba ataanza kazi kwa kupambana na uhalifu wa aina zote pamoja na ajali za barabarani. Kimsingi hayo ndiyo masuala makubwa ambayo jeshi hilo lililo na wajibu wa kulinda raia na mali zao linapaswa kuyasimamia.
Akilihutubia Taifa juzi usiku, Rais Kikwete alisema Jeshi la Polisi limeendelea kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na mafanikio yameendelea kupatikana na kusema kwamba matukio ya ujambazi yalipungua mwaka 2013 ikilinganishwa na mwaka 2012.
Alisema mwaka 2012 matukio ya ujambazi yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872 na kwa mwaka 2013 yalikuwa 6,409. Tunasema upungufu huo ni mdogo na tunaamini kwamba hiyo ndiyo changamoto kubwa inayomkabili Mangu na Kaniki katika kuwahakikishia wananchi usalama wao.
Tunasema hivyo kwa kurejea kauli ya Rais katika hotuba yake hiyo kwa Taifa juzi kwamba Julai mwaka jana, aliamua kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na utekaji wa magari katika Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma.
Tunadhani kwamba ipo haja sasa kwa Serikali kuliwezesha jeshi hilo kushika hatamu za usalama wa ndani ya nchi na kuwafanya wananchi watekeleze majukumu yao ya kila siku.
IGP Mangu pia aligusia suala la usalama barabarani. Hakuna ubishi kwamba ajali za barabarani zimekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya vifo na ulemavu kwa wananchi.
Katika hili, moja ya sababu kubwa za kuendelea kutokea kwa ajali katika mtindo unaofanana ni kutozingatiwa kwa Sheria za Usalama Barabarani, pia kutosimamiwa vyema na waliopewa dhamana.
Tunaamini kwamba kwa kuwa IGP Mangu ameliona hilo, tutaona jitihada zaidi zikiwekwa katika kuzuia ajali badala ya kusubiri zitokee ndipo hatua za zimamoto zichukuliwe. Katika hilo la ajali za barabarani, IGP Mangu anapaswa kutafuta mwarobaini wa kudhibiti ajali zinatokana na uendeshaji wa pikipiki za biashara maarufu kama bodaboda.
Licha usafiri huu kuwa mkombozi kwa wananchi hasa wa kipato cha chini, umekuwa janga kubwa kutokana na kuongeza idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani na ulemavu.
Hata hivyo, mbali na hayo, tunamtaka IGP Mangu kutupia jicho nidhamu ya baadhi ya maofisa wake hasa juu ya madai ya rushwa na kuwabambikia kesi raia.
Hivyo ni imani yetu kwamba IGP Mangu atazifanyia kazi changamoto hizo kwa kuzingatia weledi na taifa kushuhudia takwimu za uhalifu na ajali zikipungua huku malalamiko ya wananchi yaliyowafanya kupunguza imani na jeshi hilo yakitoweka.
Chanzo: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment