Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta, akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa
habari (hawapo pichani) Dar es Salaam jana kuhusu kutengwa kwa Tanzania katika nchi za Afrika
Mashariki pamoja na ‘Operesheni Kimbunga’ inayoendelea hapa nchini. Kulia ni Katibu mkuu wa
wizara hiyo Joyce Mapunjo.
habari (hawapo pichani) Dar es Salaam jana kuhusu kutengwa kwa Tanzania katika nchi za Afrika
Mashariki pamoja na ‘Operesheni Kimbunga’ inayoendelea hapa nchini. Kulia ni Katibu mkuu wa
wizara hiyo Joyce Mapunjo.
- APINGA VIKALI UTARATIBU UNAOTUMIKA KUWAONDOA
- ASEMA UNAKIUKA HAKI ZA BINADAMU, UTAWALA BORA
- AHOJI KWA MIAKA YOTE SERIKALI ILIKUWA WAPI
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,
amekosoa utaratibu unaotumika kuwaondoa wahamiaji haramu nchini kupitia
Operesheni Kimbunga, akisema ni kinyume cha haki za binadamu.Waziri Sitta amekuwa kiongozi wa kwanza nchini kukosoa
utaratibu unaotumika kuondoa wahamiaji hao tangu Rais Jakaya Kikwete, aagize
wawe wameondoka nchini ndani ya siku 14, vinginevyo wataondolewa kwa nguvu.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo
akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kagera.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sitta aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya,
jeshi la polisi na uhamiaji kuwapa muda wa kutosha wahamiaji hao ili waweze
kujiandaa kuondoka na mali zao ambazo walichuma kwa muda mrefu walioishi nchini
kuliko kuwaswagaswaga.
"Haifai kwa hawa ndugu zetu ambao
tumeishi nao kwa muda mrefu leo hii wanaswagwaswagwa jambo ambalo ni kinyume
cha haki za binadamu pamoja na utawala bora," alisema na kuongeza;"Je, Watanzania waliopo nje ya
nchi wakiondolewa kwa nguvu kama hawa wenzetu
wanavyofanyiwa tutafurahi?" Alisema kwa jambo hili Tanzania isionekane ina nongwa na nchi fulani
kwani hata Rais Kikwete, wakati anatoa agizo hilo hakusema utaratibu huo utumike.
Alitoa mfano kuwa kuna mwanamke ambaye
amefukuzwa nchini ambaye ni raia wa Rwanda
akisema aliishi kwa zaidi ya miaka 30 nchini Tanzania
na mtoto wake amesomea nchini na kuajiriwa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania
(JWTZ)."Mtu kama huyu hakutendewa
haki...mtu unamfukuza anaondoka na begi lake
moja wakati ana mali zake nyingi...huyo ni lazima arudishwe ili
ahakiki mali
zake," alisema.
Alisema walioondolewa na kuacha mali zao nyingi pamoja na watoto watarudishwa
nchini kufanyiwa uhakiki kama inavyofanyika kwa raia wa Malawi.
Alishauri wahamiaji hao watakaorudi kufuata mali
zao wapewe makazi ya muda na mali
zao zisiporwe kwani watu hao hawakuwa majambazi.
"Kama
umemuacha mtu ameishi nchini kwako kwa muda wa miaka 30 halafu leo unamfukuza
kwa kumswagaswaga nani mwenye kosa? Na muda wote ulikuwa wapi?" Alihoji
Sitta na kusisitiza kuwa; "Ndiyo maana tunasema aondolewe kwa
utaratibu."Aliongeza kuwa miongoni mwa wahamiaji
haramu waliofukuzwa baadhi yao
waliwahi kuwa viongozi wa Serikali za vijiji na mitaa katika maeneo waliyokutwa
wakiishi.
Waziri Sitta alisema tayari amepokea
barua kutoka nchi za Burundi
na Rwanda
zikilalamikia utaratibu unaotumika kuwaondoa wahamiaji haramu hao."Oktoba 1 mimi na Waziri wa Mambo
ya Ndani tutakuwa mpakani mwa Burundi na Rwanda ili kuangalia jinsi operesheni
hiyo inavyotekelezwa na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo ili
Tanzania isionekane ina malengo mabaya," alisema Sitta.
Alisema endapo utaratibu unaotumika wa kuwaondoa ukiendelea maadui
wa Tanzania
wataona njia hiyo inalenga kuwakomoa, jambo ambalo si la kweli.
0 comments:
Post a Comment