Masai Nyota Mbofu
Na Gadiel
Frank Mpungu.
Wamasai ni
moja kati ya makabila makubwa barani Afrika ambapo lenyewe lipo katika zaidi ya
nchi moja. Mavazi yao pamoja na mtindo wa kuhama hama makazi kutokana na kufuga
ni sifa zinazo zidisha umaarufu wa kabila hili.
Giliady
Severine ni mchekeshaji (comedian), kazi ambayo imempa jina kubwa hapa nchini
na kumfanya akubalike sana. Lafudhi anayoitumia msanii huyu katika kazi zake,
ni ile ya Wamasai huku akivalia na mavazi ya watu wa kabila hilo.
Giliady
ambae wengi wanamfahamu kama Nyota Mbovu au Nyota Mbofu nimzaliwa wa Ujiji,
Kigoma na kwasasa ana umri wa miaka thelathini na mitatu.
Nyota Mbovu
anasema kuwa watu wengi wanaamini kuwa yeye ni mmsai kutokana tu na kuuvaa
vilivyo uhusika wa kabila hilo. Aidha amesema kwamba si watu wa makabila
mengine tu wanaoamini kuwa yeye ni mmasai, bali hata Wamasai wenyewe wanaamini
kuwa yeye ni ndugu yao na hata kufikia hatua ya kumsemesha kilugha pindi
wamuonapo.
Mchekeshaji
huyu amethibitisha kuishia kidato cha tatu nchini Kenya mwaka 1998 na kusema kuwa
diesel
iliishia njiani na kama ingalikuwa ni meli ingalizama baharini. Baada
ya kuacha shule, Nyota Mbofu alijihusisha na uchimbaji wa madini ya Tanzanite
tangu mwaka 1998 hadi mwaka 2001.
Nyota
amesema katika maisha yake hakuna kazi nyingine yoyote anayoitegemea zaidi ya
sanaa huku Vituko sanaa group kikiwa ndicho kikundi cha kwanza kabisa Nyota Mbofu kukitumikia katika sanaa.
Katika
maongezi yake na Blog hii Giliady amekiri kuwa, aliwahi kufanya yale maonyesho
ya barabarani ambayo ameyaita kuwa ni maonyesho ya utalipa ukipenda mwenyewe, kiingilio
utajua mwenyewe.
Pamoja na
hayo amesema kwamba alishashiriki sana maonyesho ya mashuleni na kuongeza kuwa,
yalikuwa na changamoto nyingi ikiwemo wanafunzi kuja na fedha pungufu au kuja
hata na mayai au maparachichi badala ya pesa.
Mchekeshaji
huyu ambaye ameonekana kuwa mwenye furaha sana wakati akiongea na blog hii, amesema
aliamua kuigiza kimasai kwa kuwa hapakuwepo msanii yeyote aliyekuwa anaigiza
kwa kutumia lafudhi na mavazi ya kabila hilo, zaidi ya marehemu Ebo aliyekuwa
ni mwanamuziki.
Zaidi ya hilo Nyota Mbofu anasema kuwa aliona
kabila hili lipo katika nchi nyingi barani Afrika tofauti na makabila mengine
yaliyopo hapa nchini, kigezo ambacho anaamini kuwa kitamsaidia kukubalika hata
akienda huko.
Masai amesema
mpaka sasa ana nyumba ya kiasi cha shilingi milioni kumi na sita, ikiwa ni ya vyumba
viwili iliyoko Chanika, wilaya ya Temeke. Lakini kabla ya kuwa na nyumba hiyo ambayo ameiita sehemu ya kujificha, Masai
anakiri kuwa alishawahi kupata usumbufu sana katika nyumba za kupanga hususani
tangu alipoanza kuonekana kwenye runinga.
Rungu na mkuki ni nyimbo ambayo imemtambulisha
mchekeshaji huyu katika ulimwengu wa muziki ambapo amesema kuwa aliamua kuingia
katika tasnia hii ili kuzidi kuonyesha kipaji chake cha sanaa na pia
kujiongezea mashabiki. Suala ambalo amesema kwamba limefanikiwa kwa kiasi
fulani kwani hata waandaaji wa kazi zake za uchekeshaji, kwasasa wanamlipa
vizuri zaidi kutokana na umaarufu anaoendelea kujizolea katika muziki.
Vilevile Nyota
Mbofu amesema kwamba mpaka sasa ana nyimbo tatu zikiwa ni Yero suvai ambayo
amefanya na Rich Mvoko pamoja na Kitokololo, Tipwa tipwa pamoja na
nyimbo hiyo iliyomtambulisha katika muziki.
Akizizungumzia
nyimbo hizo, Giliady amesema kuwa Rungu na mkuki ni nyimbo inayo
zungumzia kazi ya ulinzi pamoja na changamoto zake.Yero suvai ikiwa ni
nyimbo inayo uelezea utamaduni wa Wamasai huku Tipwa tipwa, ikimzungumzia
mwanamke mnene na tabia zake.
Kitu
kilicho muumiza sana msanii huyu hata asikisahau ni kifo cha marehemu mama yake.
Ambapo Nyota Mbovu amesema kwamba namna alivyofikishiwa ujumbe huo haikuwa
nzuri kwani alipigiwa tu simu na kuambiwa “mama
yako kanyongwa” amesema Nyota Mbofu na kuongeza kuwa aliishiwa nguvu
ghafula na kuketi barabarani alipokuwapo wakati huo.
Kitu
kilichowahi kumfurahisha sana rafiki, ni pale alipofanikiwa kuonekana
kwenye runinga kwa mara ya kwanza, akiwa katika kikundi cha Jakaya Theatre Art.
Suala la
haki za wasanii kwa Nyota Mbofu halimuhusu sana kwani amesema kuwa hajawahi
kuwa chini ya mtu yoyote tangu aanze sanaa. Hivyo labda mpaka asimamiwe kazi
zake ndipo atajua kama wasanii hupunjwa fedha zao au ni maneno tu.
Akiliongelea
suala zima la mahusiano, Masai amesema kwamba alishawahi kuumizwa sana na
wasichana ambao wengi wao hudhani kuwa mtu kama yeye huwa na pesa nyingi,
maghorofa kadhaa na magari, jambo ambalo Masai amekiri si la kweli. Masai
aliongeza kuwa baada ya kugundua ukweli, huanza kupunguza mapenzi taratibu na kwenda
kwa wale wenye maslahi kwao.
Aidha baba
huyu wa mtoto mmoja ambaye alizaa na msichana mwenye tabia hiyo aliyoisema hapo
juu, amesema kuwa hajui ataoa lini na inatokana na yeye kuwa na bahati mbaya ya
kupata wasichana ambao si Wakristo, jambo ambalo anasema huzua utata kila
wafikiriapo suala la ndoa.
Vilevile
Nyota Mbofu ameweka wazi kwamba alishawahi kuwa na mahusiano na wa mama watu
wazima, akiwa na imani kuwa angetoka kimaisha jambo analokiri kuwa halina
ukweli ndani yake na kwamba ulikuwa ni utoto.
Giliady amesema
kuwa yeye ni mzima na ameshawahi kupima magonjwa mengi likiwemo lile la Ukimwi.
Lakini anaelezea
kwamba aliamua kupima VVU kwa mara ya kwanza kwani kwa kipindi hicho alikuwa na
mpenzi aliyesemekana kuwa muathirika. Yeye na mpenzi wake huyo walishauriana na
kuamua kwenda kupima afya zao na yeye akaonekana kuwa mzima, huku yule binti
akiwa kweli ni muathirika.
Hata hivyo
Nyota Mbovu anakiri kuwa aliumizwa sana na taarifa hizo, kwani walipendana sana.
Mchekeshai
huyu amekiri kuwa haamini kabisa katika ushirikina na kwamba yeye ni muoga sana
wa mambo hayo japo anao marafiki ambao ni waumini wazuri wa imani hizo. Giliady
anaongeza kuwa kama ingekuwa kutoka ni lazima ushiriki mambo hayo ya ushirikina,
basi yeye asingefika hata alipo sasa.
Bambo ndiye
msanii pekee anaye mvutia sana Masai ambapo mwenyewe amelithibitisha hilo na
kusema mara nyingine hata Bambo asipochekesha, huwa anacheka tu kwa kuwa
anamkubali sana.
Giliady anasema
kuvutiwa kwake huko, kulimsababisha yeye kuiiga sauti ya msanii huyo hapo
mwanzoni na hata kufikia hatua ya kuitwa Small Bambo huko mkoani Kilimanjaro.
Masai
amethibitisha kutoipenda na wala kutofuatilia kabisa siasa ya hapa nchini.
Mavazi na mtindo
wa nywele za Nyota Mbovu anasema ni tshirt na jeans kwani akivaa suruali ya
kitambaa na shati ni kama ameangukiwa na muamvuli, pamoja na rasta ambazo huamini
kwamba humpa upekee.
Matarajio
ya msanii huyu katika sanaa yake ni kuwa na nyimbo zenye mvuto zaidi kwa jamii pamoja
na kupanda kiwango katika uchekeshaji.
Vilevile
anatamani kuwa na uwezo wa kuwakusanya wasanii wa vichekesho na kufanya nao
kazi mbalimbali kama wafanyavyo sasa yeye na wachekeshaji wenzake, chini ya
kampuni moja ya hapa nchini.
Nyota Mbovu
anaomba jamii izidi kumkubali, kumfuatilia na kuzipenda kazi zake na kuongeza
kuwa anawaomba sana wasichana watoe
Ukimwi na si mimba japo hana uwakika kama utatoka, yakiwa ni maneno yake
ya mwisho kati yake nami.
0 comments:
Post a Comment