graffiti
graffiti
Na
Gadiel Frank Mpungu.
Graffiti ni moja kati ya kazi za sanaa ambayo
kwasasa imeshika hatamu katika sehemu mbalimbali duniani kote na hata nchini
kwetu pia ambapo nayo hufanya kazi zilezile za kuelimisha, kuburudisha, kuonya
na hata kupinga mambo mbalimbali katika jamii kama ilivyo kwenye sanaa zilizo
zoeleka.
Neno Graffiti kwa asili ni kutoka kule Ureno ambapo
lina maana ya mkwaruzo.Wasanii wa kipindi hicho waliokuwa wakiutumia mtindo huu
walihitaji mawe,chokaa na miti ili kuweza kuchora michoro yao na kufikisha
jumbe zao kwa jamii.
Aidha wanagraffiti hutumia mtindo ule ule wautumiao
wasanii wengine haswa wachoraji, wa kutoa mawazo akilini na kuyapeleka katika
karatasi kwa kutumia mikono yao ambapo wao huchora maumbile mbalimbali na kuandika
jumbe tofauti tofauti zenye kugusa jamii katika kuta, na si karatasi au canvas
kama wengine.
Mawazo, rangi na ukuta ndivyo vitu pekee kwasasa vinavyo
hitajika katika sanaa hii ili kufikisha ujumbe katika jamii. Rangi zinazotumika
kuchorea michoro ya graffiti hujulikana kama Spray cane (makopo ya kunyunyiza) ambapo
wataalamu wanasema kuwa rangi hizi zinaupulizaji wake ili kuweza kutoa umbile
sahihi la kitu unachotaka kukichora ukutani.
Changamoto ni zilezile kama ilivyo katika sanaa
zingine ambapo wanagraffiti wamelalamikia uhaba wa rangi ambazo ndizo muhimu
sana ili msanii aweze kufanikisha kazi yake pamoja na mambo mengine mengi likiwemo
suala zima la kukosa wateja kutokana na kile walichokiita kuwa ni kutotambulika
sana kwa kazi yao hiyo hapa nchini.
Vijana wa sasa ndilo rika pekee linaloonekana
kuvutiwa sana na aina hii ya sanaa aidha kutokana na ile imani ya usasa au
tabia ya mazoea ya kitu fulani ambayo watu wenye umri mkubwa wamekuwa nayo na
hapa wao huwa na mazoea ya aina fulani ya sanaa. Hata hivyo wasanii wenyewe wa
graffiti au waweza kuwaita wanamikwaruzo ukitumia maana halisi ya neno
graffiti, wengi ni vijana ambao kwa ujumla wao huwa na mawazo mengi akilini yakiwemo
yale ya kimapinduzi katika nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu.
Japo kuwa sanaa hii imeonekana kuwa ya kisasa zaidi
kwani hata malighafi zake hutumika zile za nje ya nchi kwa maana ya rangi,
lakini nayo inaaminika kuwa ni kati ya sanaa zenye usiri katika baadhi ya jumbe
zake zifikishwapo kwenye jamii. Usiri huo upo katika ubunifu wa michoro na maandishi
ambayo msanii huyatumia, ili kutoa yale ya moyoni ambapo kwa mara kadhaa sasa
unakuta msanii anachora michoro migumu au maneno yake kuyaandika nje ya
utaratibu uliozoeleka jambo linaloweza kuleta shida katika uelewaji wa ujumbe.
Lakini swali ni je, ni kwanini basi sanaa hii
hufanywa katika ukuta, treni, magari na sehemu nyinginezo zinazoonekana kwa
uwazi zaidi na si kwenye canvas au karatasi?
Wachata Crew ni moja kati ya makundi maarufu sana
hapa nchini katika sanaa hii ya graffiti. Aidha kundi hili lenye watu sita lililoanza
rasmi mwaka 2007, limefanikiwa kuifanya kazi hii kwa miaka sasa ambapo limejizolea
umaarufu mkubwa ndani ya nchi na hata kuipeperusha vyema bendera yetu nje ya
mipaka ya Tanzania.
Local na Kalasinga ndiyo wawakilishi wa WCT yaani
Wachata Crew Tanzania katika mahojiano yaliyofanywa na Sherehe juu ya sanaa hii,
ambapo wote walisema kuwa sanaa hii imekuwa ikifanywa ukutani na hata sehemu
nyingine za kuonekana zaidi kama kwenye treni na kwingineko, ili tu ujumbe wa
msanii uweze kufika kwa urahisi katika jamii ikiwa ni pamoja na kuonekana kwa
watu wengi zaidi.
Akifafanua kwa undani juu ya hilo, bwana Local
amesema kuwa kwenye miaka ya 1960 msanii Tack one83 ndiye aliye uanzisha mtindo
huo wa kuchora katika sehemu za uwazi na kuitambulisha vyema sanaa hii ya
graffiti kwa kutumia Spray cane kule nchini Marekani katika jimbo la Newyork,. Aidha
Local aliongeza kuwa, msanii huyo aliweza kuchora michoro mingi sana kwenye
kuta na hata kwenye treni akiwa na lengo moja kuu la kufanikiwa kuwafikia watu
wengi zaidi katika kila ujumbe aliyoutoa kupitia sanaa yake hiyo.
Hata hivyo baada ya wanagraffiti wa huko Marekani
kuonekana kuchafua mazingira na kuta za watu, serikali iliamua kuihesabia sanaa
hii kama moja kati ya makosa ya kimazingira na kuwapa adhabu wale wote
waliokutwa wakiifanya pasipo vibali rasmi vya wamiliki wa maeneo husika.
Hali hii iliwapelekea wasanii wa graffiti kwenda
mbali zaidi na kuanza kuzifanya kazi zao kwenye kuta za ndani kwa wale wamiliki
wa nyumba na maofisi waliyopenda yaani In door, ambapo kwasasa waliitumia sanaa
hii pia kama njia ya kujipatia kipato.
Hata hivyo bwana Local alipozungumzia suala la
graffiti kufanywa kwenye canvas au kuta za ndani alisema kuwa ni kuibana
graffiti kwani lengo haswa ni kuonekana kwa watu wengi zaidi pasipo gharama
yoyote ya kifedha ama muda ambao unaweza kutumika ili kwenda kuiona katika gallery
kama ilivyo kwenye sanaa nyinginezo.
Suala la uchoraji wa vitu vilivyo nje ya tamaduni na
maadili yetu au uandishi wa matusi kwa kupitia sanaa hii ni moja kati ya vitu
ambavyo WCT wakiwakilishwa na Local na Kalasinga waliweza kuviongelea pia, ambapo Kalasinga alisema
kuwa huo ni ukosefu wa nidhamu ya kazi hiyo kwani hakuna sehemu yoyote inayo
mruhusu mwanagraffiti kufanya mambo hayo.
Akiongeza juu ya hilo bwana Kalasinga alisema kuwa
jambo lingine ni ukosefu wa elimu juu ya sanaa hiyo na kuwa, watu hudhani kuwa
kila mtu anaweza kufanya graffiti na kutoa kile kilichopo akilini mwake alimradi
tu aweze kupuliza lile kopo lenye rangi jambo ambalo si sahihi kwani sanaa hii
nayo ni kazi na ina miiko kama zilivyo kazi nyingine.
Wachata pia wameliambia jarida hili kuwa ili mtu aweze
kufanya graffiti kiufundi zaidi hata iwe na ubora unaohitajika, ni lazima azingatie
mambo haya; ushikaji wa kopo,umbali kati ya msanii na ukuta,kona, kasi ya
upulizaji wa rangi(pressure), elevation pamoja na mawazo aliyo nayo aidha ya
kiburudani ama kimapinduzi.
Jarida hili pia halikuishia kwa Wachata Crew,
liliwatafuta baadhi ya wasanii ambao ni wachoraji wa michoro mingine isiyo ya
kigraffiti ili kutaka kujua zaidi sanaa hii ya graffiti wanaichukuliaje?
Jongo ni moja kati ya wasanii wakubwa ambao
wamefanya kazi nyingi sana na kuziuza sehemu mbalimbali duniani. Yeye ni
mchoraji anayetumia brush, rangi mbalimbali pamoja na canvas kama vitendea kazi
vya fani yake hiyo aliyo nayo.
Jongo amesema kuwa pia hufanya graffiti japo si
sana, lakini kwa kiasi fulani anaijua sanaa hiyo na ameshawahi kufanya kazi
mbalimbali haswa zile za ndani, kwenye kumbi za starehe(club).
Kwa upande wake Jongo amesema kuwa sanaa hii kwasasa
ndiyo inazidi kukubalika tofauti na miaka ya nyuma, na kuongeza kuwa japo kuna
changamoto nyingi sana anazopata msanii wakati akiwa anachora.
Moja kati ya changamoto hizo ni kama kudharaulika na
watu wenye umri kubwa zaidi kwa kudhani kuwa kazi hiyo ya uchoraji wa michoro
ya kigraffiti ni ya kiuni jambo ambalo amelikanusha kabisa na kusema kuwa
halina ukweli ndani yake.
Changamoto nyingine ni pamoja na ile ya gharama za
rangi hizo kuwa kubwa tofauti na rangi nyingine, ambapo yeye alisema kuwa
inamuwia vigumu sana msanii kupata ile faida inayohitajika kwani mara nyingi
wateja hulalamika bei kuwa juu wakati msanii pia anakuwa ameshatumia pesa
nyingi kuzinunua rangi hizo.
Evarist Chikawe pia ni moja kati ya wachoraji
waliyopata bahati ya kuongea juu ya mada hii ambapo yeye alikuwa na kazi ya
kuelezea jinsi wanavyoipokea aina hii ya sanaa pamoja na jinsi wananchi
wanavyoipokea kwa aonavyo.
Katika hilo bwana Chikawe ambaye pia ni msanii
maarufu hapa nchini kutokana na kufanya kazi zenye ubora na alizo ziuza katika
sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, yeye amesema kuwa kwa upande wa wasanii
wanaipokea sanaa ya graffiti kama sanaa nyinginezo ila yenyewe ikiwa ya kisasa
zaidi.
Na kwa upande wa wanunuzi yaani wananchi, bwana
Chikawe amesema kuwa nao kwasasa wameanza kuwa na uelewa wa sanaa hii japo
imechukuwa muda sana mpaka kuikubalika. Akiongeza katika hilo amesema kuwa
mpaka mtindo huo ulipofikia, uliwagharimu sana watu wenye mapenzi nao kwa
kuitangaza na hata kutoa elimu kwa jamii na hata kwa wasanii wengine ili
waipokee na kuiona kama sanaa nyingine.
Bwana Chikawe amesema kwa hapa nchini watu
waliyohusika katika mapinduzi hayo na kuipa jina sanaa hii ya graffiti, ni
Bwana Major aliyekuwa pamoja na rafiki yake wakizungu ambao kwa pamoja
walifanya workshop mbalimbali pamoja na matamasha ya kutosha ambayo yameisaidia
sanaa hii kujulikana na hata kusomeka kwenye ramani ya sanaa zinazofanyika
kwenye nchi yetu.
Katibu mtendaji, mstaafu wa Baraza la Sanaa Tanzania
(BASATA) 1978-2008, Chief Shogholo Chali naye ametoa mawazo yake kwa kadri
anavyoielewa sanaa hii.
Chief Shogholo ambaye pia kwasasa ni Director wa
Mikono Art Gallery, amesema kuwa sanaa hii kwake si ya kitambo kwani hata
alipokuwa chuoni kwenye miaka ya sabini akiwa akiwa kama mwanafuzi haikuwapo.
Kwa upande wa graffiti kuwa sanaa kama zilivyo sanaa
nyingine yeye pia amekiri kuwa ni kweli nayo ni sanaa katika upande wa
uchoraji, ambapo msanii huchukua vitu katika jamii inayo mzunguka na kisha
kuviweka akilini ambapo huvitafsiri katika namna ya kisanii na kuvirudisha
katika nammna ya michoro ambayo huiweka ukutani.
Katika sanaa hii ya graffiti, katibu huyu mtendaji,
mstaafu wa Baraza la Sanaa Tanzania ameonyesha wazi kabisa kutokuwa shabiki
nayo kwa kile alichosema kuwa inamdumaza msanii kwani anakosa ule ujuzi wa
uchanganyaji rangi kama aliyo nao msanii anayetumia canvas.
Aidha aliongeza kuwa sanaa hii hufanywa na lile rika
linalopenda vitu vya chapu chapu na urahisi urahisi ambalo ni la vijana. ”Siipendi
sanaa hii kwasababu inarahisisha kazi ya ubunifu ambayo ni sehemu ya sifa ya
usanii” aliongeza Chief.
Pia alisema kuwa sanaa hii inapunguza matumizi ya
malighafi asilia ambapo nidhahiri kuwa rangi zitumikazo hazitengenezwi kwa
kutumia mimea na malighafi zetu. Kwa kulifafanua hilo zaidi, Chief alisema kuwa
alishawahi kufanya utafiti wa rangi asilia akiwa na Profesa Jengo pamoja na
bwana Elimo Njau ikiwa ni jitihadaza kupandisha thamani, malighafi zetu katika
sanaa ya uchoraji.
Chief alipo hojiwa na jarida hili juu ya jinsi
walivyo ipokea sanaa hii kipindi alipokuwa BASATA, yeye alisema kuwa waliipokea
kwa mikono miwili huku wakiichukulia kama ni maendeleo na changamoto ambapo kwa
ujumla wake amesema kuwa waliona kama ni wimbi la kuiboresha sanaa ya hapa
nchini kwa kuileta katika mtindo wa kisasa zaidi.
Aidha aliongeza kuwa, japo kuwa sanaa hii inawadumaza
wasanii kama alivyo sema hapo awali kwa kushindwa kupata maarifa ya
uchanganyaji wa rangi katika michoro yao, lakini hawakuwa na mamlaka ya
kuipinga wala kuwakataza vijana kuifanya, kwani nchi yetu ni moja kati ya nchi
huria inayompa mtu uhuru wa kufanya biashara yoyote ile isiyo nje ya sheria,
tamaduni na maadili yetu.
Kiongozi huyu wa juu kabisa wa Mikono Art Gallery
naye ameungana kimawazo na wasanii wa graffiti na hata wale wasio wagraffiti,
juu ya tabia mbovu ya kuitumia michoro hiyo kufikisha jumbe chafu zikiwemo
matusi, jambo ambalo alisema kuwa linaweza kuwepo hata kwa wasanii ambao si
wanagraffiti.
“Sasa pamoja na kusema kuwa msanii yupo huru lakini
hayupo huru kuchinja utamaduni wetu, kwahiyo lazima vyombo vinavyo husika na
maendeleo na utamaduni vitoe miongozo itakayolinda heshima, mila na desturi za
jamii yetu” aliongeza Chief Shogholo.
Na katika upande wa maoni juu ya sanaa hii Chief
amesema kuwa hana vita na wanagraffiti wala malighafi zinazo tumika isipokuwa
tu, angetamani kama kungekuwa na uwezekano wa kuifanya kazi hiyo kwa kutumia
rangi zetu na kuongeza kuwa wasanii wanapaswa kuzifanya kazi zao kwa kuzingatia
mila na desturi huku wakitambua ya kuwa waonaji wakazi zao wapo pia watoto na
wangetakiwa wajifunze vitu kutoka kwao vyenye maadili.
0 comments:
Post a Comment