Na Gadiel
Frank Mpungu
Fatma
Binti Baraka ndilo jina alilopewa rasmi na wazazi wake, mwanamama
shujaa na mwanaharakati wa muziki wa mwambao, Bi Kidude ambaye
alizaliwa mwaka 1910.
Mwanamuziki
huyu ambaye alifikwa na umauti tarehe 17/ 4 /2013, alikuwa ni mzaliwa
halisi wa Tanzania kutoka kule visiwani Zanzibar, ambapo ndipo
alikulia huko kabla ya kuanza rasmi safari yake ya muziki ambayo
ilimtembeza katika miji mbalimbali na nchi tofauti tofauti barani
Afrika na hata nje ya bara hili.
1920,
nguli huyu wa muziki wa taarabu aliyekuwa akipinga vikali aina mpya
ya upigaji na uimbaji wa muziki huu wa mwambao kabla ya kufariki
dunia, alitoroka visiwani Zanzibar na kukimbilia katika jiji la Dar
es salaam, kutokana na kutokuwa radhi kuozwa wakati yungali kigoli wa
miaka kumi na mitatu.
1930,
mwanamama huyu aliyevutiwa na uimbaji wa mtoto wa Sultani wa
Zanzibar, Siti
binti Saad,
aliamua kuitelekeza ndoa yake baada ya mateso aliyodai kuyapata
kutoka kwa mumewe na kuamua kujiunga katika kundi la taarabu
lililojulikana kama
Egyptian Taarab group, ambalo alilitumikia kwa miaka mingi kabla ya
kurudi Zanzibar katika miaka ya 1940.
Kinara
huyu wa muziki wa mwambao pia alikuwa ni mjasiriamali
aliyejishughulisha na utengenezaji wa hina, wanja na vitu vingine
vidogo vidogo vya urembo kwa ajili ya wanawake, pamoja na kuwafunda
wasichana pindi wanapovunja ungo (unyago), kazi iliyompatia umaarufu
mkubwa kisiwani Zanzibar.
Bi Kidude akitumbuiza kwenye unyago.
Pamoja
na kuiletea heshima na sifa nchi yetu kwa zaidi ya miaka themanini,
msanii huyu mpaka anafikwa na umauti hakuwahi kumiliki nyumba nzuri
wala kuishi maisha mazuri ukilinganisha na kazi kubwa aliyokuwa
akiifanya enzi za uhai wake.
Aidha
hapakuwahi kuwepo na kitabu chochote kilichoandika juu ya maisha ya
msanii huyu iwe ndani ya tasnia, au nje ya tasnia kwa maana ya
historia yake kwa ujumla, zaidi ya makala fupi fupi kwa mfano wa hii.
Nguli
huyu aliyetamba na vibao kama muhogo wa jang’ombe,Yalaiti, Msondo
na hatimaye Ahmada, alifanikiwa kupata tunzo mbalimbali kama vile
2005 womex awards, 2012 sports and arts awards ambayo alipatiwa na
Rais Jakaya Kikwete pamoja na ile ya 2011 ya Tanzania Music Award
ambayo ilikuwa ni ya nyimbo bora ya kushirikiana (featuring song -
Ahmada) ambayo alifanya na Offside trick.
Moja
kati ya sifa alizokuwanazo mwanamuziki huyu mbobevu, ni kuweza
kuimba, kukumbuka mashahiri, kucheza ngoma, kuona vizuri, kusikia
vizuri mpaka anafikwa na umauti na kuvuta sigara tofauti na mila na
desturi za Wazanzibar na dini yake ya kiislamu.
Bi Kidude katika pozi huku akivuta sigara.
Wahenga walisema, “kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho”, hivyo mwezi
wa nne mwaka jana ndiyo ulikuwa mwisho wa safari ya mwanamuziki huyu
aliyelitikisa bara la Afrika na hata nchi za magharibi, kwa tungo
mahiri zilizobuniwa kiustadi na uweledi, ndani ya muziki wa mwambao
aliyokuwa akiufanya, kwa zaidi ya miongo minane.
0 comments:
Post a Comment